Ulimwengu ni kama robota la mitumba lililojaa vitu vya aina mbali mbali kwa jinsi ulivyosheheni aina mbali mbali za nyota.
Rangi ya nyota huwapa uwezo wana astromia kutambua uzito na jotoridi la uso wake. Nyota nzito na zenye jotoridi kali ni zile zenye rangi ya blu wakati nyepesi na za zenye jotoridi doto ni zile zenye rangi nyekundu. Hii ni kinyume na vile tulivyozoea kuwa rangi ya blu huonyesha vitu vyenye jotoridi dogo (baridi) na vyekundu huonyesha vitu vyenye jotoridi kali kama vile kwenye koki za mabomba ya maji moto na baridi.
Kama tukizipanga nyota kutoka zile zenye jororidi kali kwenda zenye jotoridi dogo, huwa tunafuata mpangilio wa makundu yafuatayo : O, B, A, F, G, K na M, ambapo nyota yetu ya Jua ipo katika umri wa katikati hivyo kuifanya iangukie katika nyota za kundi G kwenye mpangilio huu. Kama unavyoweza kuona kuwa mpangilio huu haufuati mtililiko wa silbi (alphabet), hivyo katika lugha ya Kiingereza kuna njia rahisi ya kukumbuka mpangilio huu, cha kufanya ni kukumbuka sentensi hii “Oh Be A Fine Girl/Guy, Kiss Me”. (Je unaweza kutengeneza sentensi rahisi kama hii yenye maana katika lugha ya Kiswahili ili kusaidi kukumbuka mpangilio huu? Angalia zoezi la kukusaidia chini ya habari hii).
Katika siku za karibuni timu ya kimataifa ya wanaastronomia ilichunguza nyota za aina ya 71 O ambazo zina joto kali sana kulingana na mpangilio wetu. Lakini hadi katika siku za hivi karibuni wanaastronomia walikuwa na dhana kuwa nyota nyingi za kundi O zinaishi mbali sana na nyota nyingine za jirani, ambapo utafiti mpya umeonyesha kuwa nyota 3 kati ya 4 huishi karibu sana na zile za jirani yake, na nyota 1 kati ya 3 zipo karibu sana na huweza kusababisha nyota hizo kuungana na kutengeneza nyota moja.
Kuwa mbunifu: Tungependa ututungie sentensi rahisi na yenye maana kwa Kiswahili ili itumike kukumbuka mpangilio wa makundi ya nyota, kutoka zile zenye jotoridi kali sana hadi zile zenye jotoridi la chini (O, B, A, F, G, D na M). Tafadhali tuma mawazo yako kwa info@unawe.org ukitaja na jina lako (au jina la shule kama ni kazi ya kikundi), umri na nchi.
Mponda Malozo / UNAWE-Tanzania