Sayari hii mpya iliyopo nje ya mfumo wa Jua ipo katika mfumo wa nyota tatu, uitwao mfumo wa Alpha Centauri. Hii ikimaanisha kuwa nyota hizi tatu zinazungukana. Hebu jaribu kufikiria anga linaweza kuwa na sura gani katika dunia hii ngeni!
Wanaastronomia wamegundua sayari yenye ukubwa sawa na Dunia nje kidogo ya mfumo wa Jua,ikizunguka karibu kabisa na nyota iliyo karibu nasi! Kwa mda mrefu wanaastronomia wamekuwa wakizungumzia kuhusu kuwepo kwa sayari inayozunguka nyota hii iitwayo Alpha Centauri, ambayo inafanana sana na Jua letu na pia ni sehemu ya karibu kabisa ambapo maisha yanaweza kupatikana ukiachilia mbali katika mfumo wa Jua. Ingawa miaka mingi ya utafiti ilipita bila kupata chochote, mpaka sasa.
Zaidi ya sayari 800 zimeshatambuliwa nje ya mfumo wa Jua, sayari ambazo tunaziita sayari za nje ya mfumo wa Jua “exo-planets”. Sayari hizi ni ngumu sana kuziona kutokana na kutoa mwanga hafifu unaosharabiwa na mwanga wa nyota zilizo karibu nazo. Hebu jaribu kufikiria uwezekano wa kuukamata mwanga mbele ya taa ya gari! Na kwa sababu haziwezi kuonekana moja kwa moja kwa kutumia darubini, wanaastronomia iliwabidi wawe wabunifu ili kuweza kuzitambua sayari hizi.
Njia moja ya ubunifu waliyoibuni ilikuwa ni kuangalia kwa umakini na kuona kama nyota hiyo inafifia kutokana na nguvu ya uvutano ya sayari inayoizunguka. Ili kufahamu zaidi kuhusiana na njia hii ya utafiti soma “Wobble Akiangalia Kutafuta Ulimwengu Mpya”. Hii ni njia moja iliyofanikiwa mpaka sasa katika uvumbuzi wa sayari zilizo nje ya mfumo wa Jua, ikiwamo sayari hii mpya iliyo jirani nasi na inayolingana na Dunia.
Wakati sayari hii mpya iliyogunduliwa inafanana na Dunia kwa ukubwa, ipo karibu sana na nyota inayoizunguka kuliko sayari yetu ya Dunia na pia ipo karibu zaidi kuliko hata sayari ya Zebaki, sayari ambayo ipo karibu na Jua letu. Mwaka mmoja katika sayari hiyo unaweza kuwa sawa na siku tatu tu ( ambao huo ni mda unaochukuliwa na sayari hiyo kukamilisha mzunguko mmoja wa obiti yake), wakati Dunia yetu huchukua karibu siku 365!
Ukaribu huu uliopo kati ya sayari hii na nyota unaifanya sayari iwe na joto kali sana: joto hili ni kali sana kwa ajili ya maisha kuweza kuwepo kama tunavyoyafahamu. Lakini uvumbuzi wa sayari yenye ukubwa sawa na Dunia jirani kabisa na mfumo wetu wa Jua bado ni habari ya kufurahisha sana na inatupeleka hatua moja mbele katika kutafuta maisha katika sayari nyingine.
Sayari hii mpya iliyopo nje ya mfumo wa Jua ipo katika mfumo wa nyota tatu, uitwao mfumo wa Alpha Centauri. Hii ikimaanisha kuwa nyota hizi tatu zinazungukana. Hebu jaribu kufikiria anga linaweza kuwa na sura gani katika dunia hii ngeni!
Mponda Malozo / UNAWE-Tanzania