Auroras sio mara zote huwa na rangi ya kijani, zinaweza kuwa na rangi zote za upinde wa mvua. Rangi hizi zinategemeana na umbali ambapo mwanga unaangaza tabaka la anga.
Je ushawahi kuona mwanga wa Auroras? Kama upo karibu sana na kizio cha Kaskazini au Kusini, unaweza kuona michirizi ya mwanga inayopendeza yenye rangi ya kijani ikicheza cheza angani wakati wa usiku. Watu ambao wameshuhudi husema kuwa ni moja kati ya matukio mazuri waliokwishawahi kuyaona maishani! Tukio hili la kupendeza husababishwa na chembe chembe zinazoshuka Duniani kutokea kwenye Jua, ziitwazo upepo wa Jua ‘Solar Wind’. Chembe chembe hizi hugongana na wigo wa usumaku ambapo hupelekwa kwenye vizio vya Dunia, ambapo hujipenyeza katika wigo wa sumaku na kuungana na tabaka la hewa, ambalo huzifanya kuwaka katika mwanga wenye rangi.
Katika mpaka ambapo upepo wa Jua unakutana na wigo wa sumaku pamepewa jina la ‘bow shock’. Unaweza kufananisha na kile kinachotokea wakati upanga wa meli unapokatiza kwenye maji. Kushoto katika picha, unaona bow shock ya Saturn katika rangi ya blue. Kama ilivyo kwa Dunia, Saturn ina wigo wa sumaku unaopelekea tukio la Auroras kutokea katika vizio vyake.
Chombo cha Cassini ambacho kwa wakati huu kinazunguka sayari ya Saturn, kimeshapita bow shock zaidi ya mara mia moja na kuchukua taarifa ya nguvu yake. Mpaka sasa kimekuwa kinaleta taarifa zinazofanana. Ingawa kwa wakati huu Cassini kimeleta taarifa zilizowafanya wanaastronomia kuzishangaa komputa zao kwa kutoamini. Bow shock imeonekana kuwa na nguvu mara kumi zaidi ya kawaida! Hii imesababisha chembe chembe zinazotoka katika Jua kurudishwa angani badala ya kutengeneza Auroras. Unaweza kusema Saturn imekuwa kama ngao!
Auroras sio mara zote huwa na rangi ya kijani, zinaweza kuwa na rangi zote za upinde wa mvua. Rangi hizi zinategemeana na umbali ambapo mwanga unaangaza tabaka la anga.
Mponda Malozo / UNAWE-Tanzania