Kimondo Churyumov-Gerasimenkov/67P kwa sasa kinaelekea kulifuata Jua, kikiwa katika spidi ya Km 60,000 kwa saa, hiyo ni spidi mara mbili ya vifaa vinavyoenda anga za mbali.
Juu ya Kimondo! Kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu tumefanikiwa kukitua kifaa cha anga katika uso wa Kimondo.
Baada ya safari ya miaka 10, Rosetta na Philae hatimaye ndani ya mwezi wa Agosti vimefanikiwa kufika mwisho wa safari yao katika kimondo cha 67P/Churyumov-Gerasimenko. Tangu mwezi huo Rosetta imekuwa ikizunguka na kushuka taratibu kufuata kimondo hiko, huku ikijiandaa na changamoto inayofuata ya kushusha kifaa cha Philae katika uso wa kimondo.
Kadri Rosetta ilivyokuwa inashuka katika ulimwengu huu wa ajabu, ndivyo jinsi hali ilivyozidi kuwa ya kupendeza. Tuliweza kugundua kuwa kimondo kina mabonde, milima, nyufa na kingo zenye ukubwa kama nyumba. Hata tukajua kuwa kuna milipuko ya gesi na vumbi kutoka katika uso wake.
Baada ya wiki kadhaa za kuchunguza uso wa kimondo, watalaamu walifanya uamuzi ni wapi panafaa kukitua chombo cha Philae. Baada ya uamuzi huu, kazi iliyobaki ilikuwa ni kuchagua njia bora inayozunguka kimondo ili kifaa cha Philae kiweze kutua katika sehemu sahihi.
Baada ya hapo, muda wa chombo cha Philae kukiaga chombo cha Rosetta ulifika na muda wa changamoto kubwa ya kutua pia ulifika. Jana asubuhi na mapema, Philae ilianza safari ndefu ya kutua katika kimondo, kwa muda wa masaa saba yaliyojaa hofu kubwa, tulikaa tukisubiri chombo cha Philae kilichokuwa hakiwezi kusaidiwa kushuka katika anga ya kimondo; hatukuwa na njia yeyote ya kukirudisha katika njia kama kingetoka nje.
Mwisho kabisa, tulipata ahueni kubwa na kupiga makofi, tulipo pokea neno kutoka katika chombo cha Philae kuwa kimefika salama na kimefanikiwa kujishikiza vyema!
Tayari chombo cha Philae kimeanza kuchukua taarifa kwa kadri kiwezavyo kuhusu Dunia hii ndogo, pamoja na Rosetta ambayo inazunguka kwa karibu juu ya kimondo. Vifaa hivi vitatusaidia kuwa na uelewa wa moja kati ya mada kongwe zaidi katika mfumo wa Jua.
Kimondo Churyumov-Gerasimenkov/67P kwa sasa kinaelekea kulifuata Jua, kikiwa katika spidi ya Km 60,000 kwa saa, hiyo ni spidi mara mbili ya vifaa vinavyoenda anga za mbali.
Mponda Malozo / UNAWE-Tanzania